Mataifa ya Afrika ya Kati yamteua mwenyekiti mpya wa tume ya ECCAS kutoka Burundi


Tume ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati ina rais mpya. Wakuu wa nchi za ECCAS waliokutana siku ya Jumapili, Septemba 7, huko Sipopo, Equatorial Guinea, wamemteua Balozi wa Burundi na waziri wa zamani wa mambo ya nje, Ézéchiel Nibigira, kushika nafasi hii. Ataongoza tume hii kwa miaka mitano ijayo. Anamrithi Gilberto Verissimo kutoka Angola, ambaye uongozi wake umekosolewa pakubwa.
Haya ndiyo yalikuwa matokeo makuu ya mkutano wa kilele wa Septemba 7 wa ECCAS, Tume ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika ya Kati: mabadilikokatika uongozi wa Tume ya jumuiya hiyo. Ézéchiel Nibigira ambaye ana shahada ya udaktari katika usimamizi wa biashara na fedha, ni kiongozi katika chama cha rais wa Burundi CNDD-FDD.
Ameshikilia nyadhifa maarufu kwa takriban miaka ishirini: rais wa umoja wa vijana wa chama chake, mbunge, balozi nchini Kenya, waziri wa mambo ya nje, na kisha waziri mwenye dhamana ya EAC (Jumuiya ya Afrika Mashariki) hadi mwezi Julai mwaka huu.
Kazi ngumu
Akiwa amechaguliwa tena kuwa mbunge, sasa anachukua uongozi wa Tume kwa kipindi cha miaka mitano. Mara moja wakuu wa nchi wamemwapisha. Lakini kazi yake inaonekana kuwangumu. Atalazimika kurejesha uaminifu wa Tume iliyokosolewa haswa kwa usimamizi wake, kuendeleza mchakato wa mageuzi ya kitaasisi uliozinduliwa mwaka 2015, na zaidi ya yote, kufuatilia kwa karibu hali ya usalama katika eneo hilo, hasa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kazi nyeti, ikizingatiwa kwamba nchi yake, Burundi, mshirika wa DRC, inadumisha uhusiano mbaya na Rwanda. Kigali pia ilijiondoa katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (ECCAS), ikiishutumu msimamo wake usiyoyumba kwa kuiunga mkono Kinshasa. Wakati wa mkutano wa kilele wa Septemba 7, viongozi walipokea ripoti ya usalama na hali ya kibinadamu kuhusu mgogoro wa mashariki mwa DRC, ambapo maeneo kadhaa yanaendelea kuwa chini ya udhibito wa kundi lenye silaha linaloungwa mkono, wanasema, kutoka nje.
Comments are closed.