Sudan yaomba msaada baada ya maporomoko ya udongo kuua zaidi ya 1,000 Tarasin

335
kwibuka31

Sudan imeomba msaada wa kimataifa siku ya Jumanne baada ya maporomoko ya ardhi kuharibu kijiji kizima katika mkoa wa Darfur magharibi, na kuua karibu watu 1,000 katika moja ya maafa mabaya zaidi ya asili katika historia ya hivi karibuni ya nchi hiyo ya Afrika.

Kijiji cha Tarasin “kimeharibiwa kabisa,” limesema vuguvugu la Ukombozi wa Sudan (SLM-Army), ambalo limetoa wito kwa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu kwa msaada wa kutafuta miili ya watu waliofariki.

Mkasa huo ulitokea siku ya Jumapili katika kijiji hicho, kilichoko kwenye Milima ya Marrah katikati mwa Darfur, baada ya siku kadhaa za mvua kubwa.

“Ripoti za awali zinaonyesha vifo vya wakaazi wote wa kijiji hicho, zaidi ya watu 1,000,” kundi la waasi lmesema katika taarifa yake. “Ni mtu mmoja tu aliyenusurika,” limeongeza.

Abdel-Wahid Nour, kiongozi wa kundi hilo, ameomba msaada wa kimataifa siku ya Jumanne. “Kiwango na ukubwa wa maafa ni makubwa na hayaelezeki,” amesema.

Baraza tawala la Khartoum limeomboleza vifo vya mamia ya wakaazi wasio na hatia kufuatia maporomoko ya ardhi katika milima ya Marrah. Katika taarifa, limesema kwamba “uwezo wote unaowezekana” umehamasishwa kusaidia eneo hilo.

Picha zilizotangazwa na vyombo vya habari vya Milima ya Marrah zilionyesha eneo tambarare kati ya safu za milima, huku kundi la watu likifanya upekuzi kuwatafuta manusura au miili ya watu waliofariki.

Luca Renda, mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Sudan, amesema “amehuzunishwa sana” na maporomoko ya ardhi yaliyoripotiwa, akiongeza kuwa vyanzo vya ndani vinaonyesha kuwa “kati ya watu 300 na 1,000 wanaweza kuwa wamepoteza maisha.” Amesema Umoja wa Mataifa na washirika wake wanahamasishwa kusaidia jamii zilizoathirika katika kijiji hiki.

Mtandao wa dharura wa eneo hilo, ambao unatoa msaada kwa jamii kote Sudan wakati wa vita, umesema timu zake zimepata miili ya watu tisa siku ya Jumanne. Timu za watafutaji zilitatizika kufika eneo hilo kutokana na hali mbaya ya hewa na ukosefu wa rasilimali, ameongeza.

Comments are closed.