Ubelgiji yatangaza kulitambua taifa la Palestina kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa

289
kwibuka31

Ubelgiji italitambua taifa la Palestina katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Maxime Prévot ametangaza leo Jumanne, Septemba 2, akiungana na nchi zingine kama vile Ufaransa na Canada.

Palestina itatambuliwa na Ubelgiji katika kikao cha Umoja wa Mataifa! Na vikwazo vikali vinawekwa dhidi ya serikali ya Israel,” ameandika waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Mwishoni mwa mwezi Julai, Rais Emmanuel Macron alitangaza kuwa Ufaransa italitambua taifa la Palestina kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, utakaofanyika kuanzia Septemba 9 hadi 23 mjini New York. Kufuatia hayo, zaidi ya serikali kumi na mbili za Magharibi zilitoa wito kwa nchi nyingine duniani kufanya hivyo.

“Ubelgiji itajiunga na nchi zilizotia saini Azimio la New York, kufungua njia kuelekea suluhisho la serikali mbili na kwa hivyo kuzitambua,” waziri Maxime Prévot ameelezea.

Masharti na vikwazo

Lakini utambuzi huu wa taifa la Palestina unasalia chini ya masharti: utarasimishwa tu wakati “mateka wa mwisho atakapoachiliwa na Hamas haitachukua tena jukumu lolote la usimamizi wa Palestina,” Maxime Prévot alielezea kwenye X.

Waziri huyo pia ametangaza vikwazo kumi na viwili dhidi ya Israel. Hivi ni pamoja na “marufuku ya uingizaji wa bidhaa kutoka kwa makazi ya Waisrael,” pamoja na “mashitaka ya kisheria yanayowezekana, marufuku ya kusafiri kupita kiasi na usafirishaji, na kujumuishwa kwa mawaziri wawili wa Israel wenye msimamo mkali, walowezi kadhaa wenye jeuri, na viongozi wa Hamas kwenye orodha ya ‘watu wasiotakiwa’ katika nchi yetu.

Robo tatu ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa tayari wamelitambua taifa la Palestina

Uamuzi huu uko mbali na kuungwa mkono kwa kauli moja ndani ya serikali ya Ubelgiji, huku wanachama kutoka vyama vya mrengo wa kulia N-VA na MR wakionyesha kusitasita. Hata hivyo, “kutokana na maafa ya kibinadamu yanayotokea Palestina, hasa huko Gaza, na katika kukabiliana na ghasia zinazofanywa na Israel kinyume na sheria za kimataifa […], Ubelgiji imebidi kuchukua maamuzi makali ili kuongeza shinikizo kwa serikali ya Israel na magaidi wa Hamas,” Waziri wa Mambo ya Nje amebainisha.

Canada na Australia tayari wameelezea nia yao ya kuungwa mkono kuundwa kwa taifa la Palestina. Uingereza pia ilitangaza kuwa italitambua taifa la Palestina isipokuwa Israel itatoa misururu ya ahadi, ikiwa ni pamoja na kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza. Kwa jumla, robo tatu ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanalitambua taifa la Palestina, lililotangazwa na uongozi wa Palestina uhamishoni mwaka 1988.

Comments are closed.