Faida za kiafya kwa wanawake wenye makalio makubwa

28,079

Licha ya mvuto yaliyonayo yakiwa kwenye jinzi, makalio makubwa ya wanawake ni kinga kwa kisukari na magonjwa ya moyo.

Wataalamu wa afya wanadokeza kwamba makalio ni muhimu kwa afya ya binadamu kwani huwezesha kusimama na kutembea vile anavyoonekana. Na cha pekee, hueleza afya ya mtu hasa mwanamke.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza unaeleza uhusiano uliopo baina ya mwonekano wa makalio ya mwanamke na hatari yake ya kupatwa na magonjwa hayo kwa kuzingatia mgawanyo wa mafuta mwilini.

Majibu ya utafiti huo yanaeleza kuna uhusiano wa karibu kati ya mgawanyo wa mafuta mwilini na afya ya mwanamke ingawa mafuta hayo hayasambazwi kwa usawa kwenda sehemu tofauti za mwili.

Kiasi kikubwa cha mafuta kikihifadhiwa kwenye matiti ni hatari kwa afya kwa sababu yapo karibu na moyo kwani huongeza uwezekano wa kuziba kwa mishipa ya damu, lakini makalio ya wastani yanaashiria siha njema.

Utafiti huo ulibaini uvungu wa makalio hasa sehemu za juu za mapaja na nyonga ndiko yanakohifadhiwa mafuta ya ziada au fatty acids ambayo ni kinga dhidi ya magonjwa hivyo mhusika kuwa na afya njema.

“Mafuta yasipohifadhiwa sehemu salama huenda kwenye ini au mishipa ya damu ambako huweza kusababisha kisukari au magonjwa ya moyo,” anasema Dk Konstantinos Manolopoulos, kiongozi wa utafiti huo.

Ipo tofauti kati ya mwanamke na mwanaume kuhusu usambazaji wa mafuta mwilini.

Inaelezwa kwamba wanawake wanahifadhi zaidi mafuta sehemu ya chini ya mwili; mapaja, nyonga na makalio kuliko wanaume.

Hii ni habari njema kwa wanawake na wasichana ambao bado wanapata siku zao kwani kwa mujibu wa Dk Manolopoulos, kuwa mwanamke mwenye homoni za kike ni kinga ya magonjwa ya moyo kwa kiasi fulani. Lakini baada ya kukoma kwa hedhi, homoni hubadilika.

“Mwonekano wa kike unapotea na badala yake kitambi huanza kujitokeza. Badala ya mafuta kwenda makalioni, sasa yanahifadhiwa tumboni hivyo kuongeza uwezekano wa kupata maambukizi ya magonjwa hayo hivyo kuwa sawa na wanaume wa umri huo,” anasema huyo.

Utafiti wa awali uliofanywa mwaka 2008 na kuchapishwa kwenye International Journal of Obesity kwa kutumia panya ulionyesha kwamba licha ya mafuta yanayohifadhiwa tumboni kuyeyushwa kwa urahisi, ni hatari kwani huziba mishipa ya damu na kurahisisha mshtuko wa moyo.

Ingawa hakuna uhakika wa namna mwili unavyogawanya hifadhi ya mwilini, watafiti hao wanabainisha kwamba watu wenye makalio makubwa wana nafasi ndogo ya kupata maradhi hayo hata watakapozeeka.

Dk Benjamini Rulakuze wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), anasema unaunga mkono utafiti huo na kufafanua kuwa magonjwa ya moyo na kisukari husababishwa na wingi wa mafuta katika mwili.

Dk Rulakuze anasema sehemu za tumbo, matiti, mapaja na makalio ndiyo hutumika zaidi kuhifadhi mafuta kwa mwanamke na endapo mtu atakuwa na mafuta mengi yanaweza kuathiri mishipa ya damu kwani hurundikana na kuifanya mishipa ya damu kuwa miembamba na kuzuia damu kupita kwa urahisi hali inayorahisisha shinikizo la damu.

Anasema: “Mafuta huathiri ufanisi wa kongosho kuzalisha homoni ya insulini ambayo hutumika kusafirisha sukari ya mwili kwenda kwenye seli za mwili ili zitumike kuupa mwili nguvu.”

Anasema endapo sukari itashindwa kuingia katika seli za mwili na kuyeyushwa, mtu anaweza kupata kisukari aina ya kwanza na ya pili.

Na endapo mafuta yatakuwa mengi yanaweza kubadili oksijeni iliyokuwa itumike kusafirisha glucose na kufanya seli zishindwe kupokea sukari hiyo, hivyo kuibakiza sukari kwenye damu na kusababisha ongezeko la sukari katika damu.

Daktari huyo anaeleza kuwa mbali na wanawake, wanaume ambao hupata matatizo ya kisukari na magonjwa ya moyo ni kutokana na mafuta mengi katika tumbo na kusababisha kitambi ambavyo wengi wetu hudhani kuwa ni afya.

“Endapo mafuta hayo yataongezeka zaidi huathiri mfumo wa damu kwa kuziba mishipa hivyo kuinyima nafasi ya kutosha kupita na kusababisha shinikizo la damu,” anasema.

Anaeleza kuwa ili kuepukana na matatizo hayo ni vema mtu akafanya mazoezi kila wakati ili kujiweka sawa na kupunguza mafuta mwilini. Mazoezi hayo yanaweza kuwa ni kukimbia, kukata tumbo na mengine ambayo husaidia kupunguza mwili.

Mbali na mazoezi ameshauri kuwa makini na matumizi au ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi kama nyama na kupendekeza matumizi ya mafuta ya mimea.

Daktari mwingine, Eliza Wampembe wa Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili (Muhas) anasema mbali na sababu hizo, kisukari kinaweza kurithiwa kutoka kwa wazazi au wanafamilia wengine ambao walikuwa na ugonjwa huo ndani ya ukoo.

Dk Eliza anabainisha kuwa mgonjwa wa moyo na kisukari yupo hatarini kuathirika na maambukizi mengine kwani huathiri figo na kongosho, hivyo kupunguza kinga za mwili.

“Miongoni mwa athari za kisukari ni miguu kuwa na vidonda visivyopona kwa urahisi kiasi cha kukatwa kwa baadhi ya wagonjwana kusababisha ulemavu ambao hawakuzaliwa nao,” anasema.

Pia, shinikizo la damu husababisha matatizo ya figo, macho, kiharusi, misuli ya tumbo na kutosikia vizuri.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2015 ya Shirikisho la Kisukari (IDF) Afrika, zaidi ya watu milioni 14 barani humo wana ugonjwa huo na idadi inaweza kuongezeka hadi kufikia milioni 34 mwaka 2040 endapo jitihada za dhati za kukabiliana nao hazitachukuliwa.

Ripoti hiyo inasema asilimia 66.7 ya watu wote barani Afrika wana kisukari, kati yao asilimia 79 ni wenye umri zaidi ya miaka 60.

Ripoti imeeleza ugonjwa huo ulisababisha zaidi ya vifo vya watu 300,000 mwaka 2015.

Licha ya mikakati ya Serikali kukabiliana na magonjwa mbalimbali, wataalamu wa afya wanashauri kila mwananchi kuwa makini na kuchukua tahadhari zinazotolew.

Comments are closed.